MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) unatarajia kuanza rasmi leo Jumamosi kwa mechi takribani saba.Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, wataanzia nyumbani kwenye ng’we hiyo, kwa kumenyana na Ndanda mchezo utakofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.
Azam FC ilimaliza vema raundi ya kwanza ya ligi, baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 30 katika nafasi ya pili kufuatia ushindi wa mechi nane, sare sita na kupoteza mchezo mmoja pekee dhidi ya Yanga (2-1) ikizidiwa pointi tano na kinara Simba aliyejizolea 35.
Kama hiyo haitoshi, matajiri hao wa viunga vya Azam Complex ni miongoni mwa timu mbili bora zilizofungwa mabao machache kwenye ligi hiyo mpaka sasa, nyingine ikiwa ni Simba, zote zikiruhusu nyavu zao kutikiswa mara sita tu katika mechi 15 zilizochezwa.
Mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Kombe la Mapinduzi, wako kwenye hali nzuri kuelekea mchezo huo dhidi ya Ndanda, wachezaji wakiwa na morali ya hali juu baada ya Jumanne iliyopita kutoka kuichapa Shupavu ya Morogoro mabao 5-0 na kufuzu hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).
Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, ameshaweka wazi kuwa amejipanga kushinda mchezo huo na kuendelea kupambana kuhakikisha timu hiyo inaipiku Simba katika mbio za ubingwa wa ligi hiyo.
“Mashabiki wa Azam FC wanatakiwa kujua kuwa mawazo yangu kama kocha, sitarudi nyuma, nimecheza mpira huko nyuma na katika kichwa changu nimekuwa nikipenda kushinda kila wakati.
“Nimeona baadhi ya watu baada ya mechi na Yanga wamekuwa wakidhani kuwa timu ya Azam itarudi chini lakini napenda kuongea na kila mtu kuwa timu hii haitaenda chini na itapambana kwa ajili ya nafasi ya kwanza,” alisema Cioaba siku chache zilizopita wakati kikosi hicho kikianza maandalizi ya kuikabili Ndanda.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, Maji Safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, itaingia kwenye mchezo huo ikiwakosa nyota wake, nahodha Himid Mao ‘Ninja’, kiungo Stephan Kingue, mshambuliaji Wazir Junior, ambao ni majeruhi.
Aidha itamkosa kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye atakuwa akitumikia adhabu yake ya kukosa mechi moja baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu iliyotokana na kadi mbili za njano kwenye mchezo uliopita dhidi ya Yanga.
Huo utakuwa ni mchezo wa nane kwa Azam FC kukutana na Ndanda kwenye ligi, matajiri hao wakiwa vinara baada ya kuwachapa wapinzani wao mara nne, Ndanda ikishinda mbili na mechi zikienda sare, ambayo ndiyo ilikuwa mechi pekee kwa timu hiyo yenye maskani yake mkoani Mtwara kuvuna pointi ndani ya viunga vya Azam Complex kufuatia sare ya mabao 2-2.
Katika mechi hizo saba walizocheza, jumla ya mabao 12 yamefungwa, Azam FC ikitupia saba kwenye nyavu za Ndanda huku ikiruhusu mabao matano kutoka wapinzani wao hao, ambao kwenye msimamo wa ligi wanashika nafasi ya nane wakiwa na pointi 16.Itakumbukwa kuwa katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Azam FC ilishinda bao 1-0 ugenini, lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Yahaya Mohammed kutoka nchini Ghana.
Comments