www.ngwenjetv.wixsite.com/news
HALI ya Tanzania kuibuka kinara miongoni mwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuwa na uchumi jumuishi, inatokana Serikali kujipanga vizuri katika maeneo sita, ikiwemo kuwa na miundombinu bora, huduma bora za kifedha, kupambana na rushwa, ujasiriamali, elimu na afya bora.
Aidha, nchi hiyo imepata ushindi huo kutokana na kuwa na sera na sheria zinazowaleta watu wengi katika uchumi jumuishi, kama vile sheria mpya ya madini na sheria ya simu. Hayo yalibainishwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa, wakati akizungumza na waandishi wa habari wa magazeti ya Tanzania Standard Newspapers (TSN) na Idara ya Habari (Maelezo) Dar es Salaam jana.
Alisema Tanzania imekuwa na uchumi jumuishi kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Word Economic Forum (WEC) kupitia mradi wake wa The Inclusive Development Index jambo ambalo Watanzania wanapaswa kujivunia na kutobweteka, bali wachape kazi zaidi.
Alielezea sababu za vigezo hivyo kuipatia ushindi Tanzania katika eneo hilo la uchumi jumuishi kuwa vimeiwezesha nchi hiyo kujiweka imara katika eneo zima la kukuza uchumi kuanzia ngazi zote za taifa Aidha, alisema katika rushwa, tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupambana na kudhibiti rushwa jambo lililotoa fursa hadi kwa mwananchi wa ngazi ya chini kupata huduma bila kupata vikwazo vya rushwa.
“Tanzania imefanikwa sana katika eneo la huduma yafedha. Kwa sasa nchi hii imetajwa kufanya vizuri kwa kuwa na benki nyingi ikilinganishwa na nyingine za Afrika,” alisema Issa. Alisema pamoja na utitiri wa benki pia kupitia kampuni za simu ambazo kwa sasa zinatoa huduma za fedha kupitia mtandao wa simu, takribani asilimia 95 ya Watanzania wanapata na kufikiwa na huduma za kifedha.
Katika kigezo cha umiliki wa biashara na wajasiriamali, Katibu Mtendaji huyo alisema nchi imefanikiwa kuboresha eneo hilo kwani hivi karibuni ilizindua mkakati wa wajasiriamali wenye lengo la kutoa muongozo wa kukuza ujasiriamali nchini. “Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa kuna wafanyabiashara wanaofikia milioni tatu kila mwaka wengi wao wakiwa ni wa chini.
Ingawa hawa wengine biashara zao zinakufa, ukweli unabaki kuwa wengi wanafanikiwa kuendeleza biashara zao… inaonesha kuwa sera zetu ni nzuri kiuchumi,” alieleza. Akizungumzia kigezo cha afya na elimu, alisema sera ya elimu bure na huduma bora za afya ikiwemo suala la bima ya afya ni moja ya sababu iliyoipa ushindi Tanzania katika eneo hilo la uchumi jumuishi.
Issa pia alizungumzia kigezo cha hifadhi ya jamii na kufafanua kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeboresha sera ya hifadhi ya jamii kwa kuweka mifuko miwili itakayosimamia sekta binafsi na ya umma ambayo nayo imekuja na ubunifu wa namna ya bora ya kuwafikia na kuwawezesha wananchi.
Alisema baraza la uwezeshaji ambalo kazi yake kubwa ni kusimamia sera za uwezeshaji kiuchumi, limefanya kazi kubwa ya kutangaza sera na mipango maalumu ya kuhakikisha wananchi wote wanashiriki kiuchumi. Alisema baraza hilo limejipanga kuhakikisha baada ya miaka mitano, liwe limewafikia wananchi na kuwashirikisha na kuwawezesha kiuchumi.
“Tunataka Watanzania wanufaike na uwekezaji wowote unaofanyika nchini,” alisema. Alisema hali hiyo ndiyo iliyoisukuma NEEC kuingia mkataba na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA) ili kuhakikisha Watanzania wanashiriki na kunufaika na manunuzi ya umma badala ya kampuni au mashirika ya nje pekee. Pamoja na Katibu huyo, wadau wengine waliozungumza na gazeti hili kuhusu ushindi huo kwa Tanzania, walisema, kwa kiasi kikubwa unachangiwa na jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali kukuza uchumi.
Pamoja na mafanikio hayo, Issa alitaja changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi ili nchi hiyo ifanye vizuri zaidi kuwa ni kutokuwepo kwa uratibu mzuri wa taarifa za masoko na Watanzania kuongezewa ari ya kushiriki katika uchumi. Alisema katika eneo hilo, serikali ina mkakati maalumu wa kufundisha ujasiriamali kuanzia shuleni. Alitaja changamoto nyingine kuwa ni mitaji ambapo bado taasisi nyingi za fedha zinatoa mikopo yenye masharti magumu.
Hata hivyo, alisema pamoja na mafanikio hayo, baraza hilo halitojibweteka na litajitahidi kufanya vizuri ili kuiwezesha Tanzania kufanya vizuri zaidi kiuchumi. Mbali na Katibu Mtendaji huyo, wadau wengine walisema hatua ya Tanzania kuibuka kinara kwa kuwa na uchumi jumuishi inachangiwa na jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali kukuza uchumi.
Mkurugenzi EPZA Mkurugenzi wa Eneo la Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) nchini, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia, alisema ujenzi wa miundombinu mipya na kuboresha iliyopo kwa kiasi kikubwa umewezesha Watanzania wengi kuanzia mijini hadi vijijini kuendesha kirahisi shughuli zao za kukuza uchumi, hatua inayoifanya Tanzania kuendelea kufanya vizuri.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka, alisema katika miaka ya karibuni, kumekuwa na ushirikishwaji wa moja kwa moja wa wananchi katika kuendesha shughuli mbalimbali zikiwemo za uanzishaji wa viwanda, na hivyo kuwasaidia kukuza uchumi. Mtaka alisema Tanzania imezidi kujiweka vizuri katika kutengeneza mazingira ya wananchi kushiriki kwa pamoja katika kutengeneza uchumi wao, tofauti na ilivyo kwa mataifa mengine ambapo sehemu kubwa ya ukuzaji uchumi huendeshwa katika mfumo wa kibepari.
“Serikali pia inajenga uchumi ambao kila mwananchi anashirikishwa kikamilifu, ukiangalia yote ambapo kuna kichocheo cha uchumi, unaona kabisa wananchi wa ngazi zote kuanzia juu mpaka chini, wanashiriki kuujenga, hatua inayomfanya kila mmoja kujiona sehemu ya ujenzi wa uchumi huo,” alisema Mtaka. Pamoja na sababu nyingine, alisema uwepo wa benki maalumu zinazohusika na kilimo, kwa kiasi kikubwa umewawezesha wananchi kupata mitaji.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alisema mabadiliko yaliyopo kwenye uchumi jumuishi yanatokana na jinsi viongozi na watumishi wa serikali wanavyosikiliza wananchi.
Alisema, “Wananchi wamekuwa na changamoto nyingi, lakini pia wana mawazo mengi mazuri, wanaposikilizwa na kushirikishwa wanachangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ambayo ni mazuri kwa taifa. “Cha msingi tusibweteke kwa kusifika kuwa kwenye nafasi nzuri kwenye uchumi jumuishi, tunatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kuwasikiliza wananchi,” alisema Mghwira.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe alisema kupitia uchumi Jumuishi, katika msimu uliopita, ekari 700,000 za ardhi zilizalishwa na kuzaa ajira zipatazo 100,000 hatua aliyosema imechangia mkoa huo kuwa na tija. “Hii imewezesha mkoa kuwa na rekodi nzuri ya chakula cha ziada kwa sababu wakulima wanaweza kukopa matrekta katika vikundi vidogo... hatua inayomaanisha utekelezaji wa vitendo wa sera za uchumi jumuishi.
Alisema mkakati wa sasa wa mkoani humo ni kuhamasisha vijana kushiriki vizuri katika kilimo ili kuongeza fursa kwa vikundi mbalimbali kushiriki katika uchumi wa kitaifa. Katika orodha ya nchi 10 bora, nchi zilizofuatia za Afrika na nafasi zilizoshika kidunia ni pamoja na Ghana (52), Cameroon (53), Burundi (55), Namibia (56), Rwanda (57), Uganda (59), Mali(60), Senegal (61) pamoja na Nigeria iliyoshika nafasi ya 63.
Comments