MAKAMU Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Pius Msekwa amesema kuwa ushindi ulioupata CCM kwenye uchaguzi uliofanyika jana ni ishara nzuri kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.Msekwa alisema kuwa ingawa kitendo cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia uchaguzi huo kinafifisha demokrasia ya vyama vingi, bado hata kama vingeshiriki CCM ingeshinda tu.
Alisema kitendo cha Ukawa kususia uchaguzi huo ndiyo sababu ya CCM kupata ushindi mkubwa kwa kuwa vyama vidogo visingeweza kuwa kikwazo kwa ushindi wa kishindo wa CCM.
“Ni ushindi mzuri na halali kwa CCM, kwa kuwa kujiondoa kwa Ukawa hakuathiri ushindi kwa CCM. Hata kama Ukawa wangeshiriki, bado CCM ingeshinda, sema tu labda zile asilimia za ushindi zingepungua kidogo,” alieleza Msekwa.
Alisema ushindi huo wa CCM ni dalili nzuri kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Alisema kama upinzani wataendelea na tabia ya kususia uchaguzi maana yake ni kwamba CCM itaendelea kupata ushindi wa kishindo, ingawa itaondoa hali ya ushindani na kuwa kama enzi za chama kimoja.
Msekwa alisema hayo kufuatia CCM kuibuka kidedea kwa ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo matatu ya Longido, Singida Kaskazini na Songea Mjini.
Kwenye Jimbo la Longido lililopo mkoani Arusha, Dk Stephen Kiruswa alitangazwa kuwa mbunge wa Jimbo hilo baada ya kupata kura 41,258 na kuwaacha kwa mbali wagombea wanzake wanane waliokuwa wakiwania kiti hicho.
Naye Justin Monko aliibuka kidedea kwenye Jimbo la Singida Kaskazini baada ya kuibuka mshindi kwa kura 20,857, sawa na asilimia 93.5 ya kura 22,298 zilizopigwa. Mwanasheria maarufu nchini, Dk Damas Ndumbaro amekuwa mshindi wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Songea Mjini, kwa kupata kura 45,762 sawa na asilimia 97 ya kura zote.
LONGIDO
Dk Kiruswa alipata ushindi huo wa kishindo ambao ni sawa na asilimia 99.1 kati ya kura 41,744 zilizopigwa katika Jimbo hilo la Longido lenye wakazi wengi wa jamii ya kifugaji.
Majira ya saa 3:45 asubuhi jana, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Juma Mhina, alimtangaza Dk Kiruswa kuwa mshindi akisema, “Kwa mamlaka niliyopewa na Tume Taifa ya Uchaguzi (NEC) ninamtangaza Dk Kiruswa mgombea wa CCM kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi katika Jimbo la Longido kwa kupata kura 41,258 sawa na asilimia 99.1.” Mhina alisema katika uchaguzi huo wananchi waliojitokeza kupiga kura ni 41,744 sawa na asilimia 72 ya wapiga kura 57,808 waliojiandikisha.
Msimamizi huyo alitaja wagombea wengine walioshiriki uchaguzi huo na kura zao kuwa ni pamoja na Mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Kisiongo Ole Kurya aliyepata kura 163 sawa na asilimia 0.39.
Godwin Sarakikya wa Ada Tadea aliyepata kura 60 sawa na asilimia 0.14, Francis Ringo kutoka CCK aliyepata kura 47 sawa na asilimia 0.11 na mgombea wa TLP, Robert Lukumay aliyepata kura 36 sawa na asilimia 0.11.
Wengine aliowataja ni mgombea wa AFP, Mgina Ibrahimu Mustafa aliyepata kura 34 sawa na asilimia 0.08. Ngilisho Simoni Poul mgombea wa Chama cha Demokrasia Makini ambaye alipata kura 14 sawa na asilimia 0.03,mgombea wa SAU Saimoni Bayo alipata kura 13 sawa na asilimia 0.03 na mgombea wa Chama Cha NRA, Feruziy Ferusiyson aliambulia kura 9 sawa na asilimia 0.02.
Baada ya kutangazwa mshindi wa ubunge katika jimbo hilo, Dk Kiruswa aliwashukuru wana Longido kwa kumpa kura hizo za kishindo na kuahidi kuleta maendeleo Longido. Dk Kiruswa alisema wananchi wa Longido wamekaa zaidi ya miaka miwili bila kuwa na mwakilishi bungeni na kwamba, atafanya kila linalowezekana kuhakikisha anatatua changamoto zinazolikabili jimbo hilo kwa kadri inavyowezekana.
Mbunge mteule huyo anashinda baada ya uchaguzi huo kurudiwa kufuatia maamuzi ya mahakama kutengua ushindi wa mwaka 2015 wa mgombea wa Chadema, Onesmo Ole Nangole aliyedaiwa kukiuka baadhi ya sheria za uchaguzi.
Mgombea wa NRA, Feruziy Juma Feruziyson na mgombea wa SAU, Saimon Bayo, walisema wana Longido hawakufanya makosa kumchagua Dk Kiruswa kwani mgombea huyo wa CCM ni dhahabu kwa wananchi wa Jimbo hilo.
Walisema wanachotakiwa wana Longido kuwa wamoja kwani uchaguzi ulishamalizika na kinachohitajika ni ushirikiano wa dhati wenye kumtumia vema Kiruswa kuipaisha Longido kuwa wilaya ya mfano kwa maendeleo ya wilaya zote za kifugaji.
Bayo alisema mara zote ukiwa unashindana unapaswa kukubali matokeo na kumkubali aliyeshinda kwani hiyo ndiyo demokrasi ya kweli, badala ya kupinga kila kitu kwani siasa za namna hiyo zimeshapitwa na wakati.
SINGIDA KASKAZINI
Mrithi wa Lazaro Nyalandu katika Jimbo la Singida Kaskazini amepatikana baada aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya (DED) ya Liwale mkoani Lindi, Justin Monko kuibuka mshindi kwa kura 20,857 sawa na asilimia 93.5 ya kura 22,298 zilizopigwa.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo mdogo jana, Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo hilo, Rashid Mandoa alisema zaidi ya asilimia 75 ya wapiga kura 91,562 walioandikishwa kupiga jumla hawakujitokeza kwenye zoezi hilo.
Mandoa aliwataja wagombea wengine waliokuwa kwenye kinyang’anyiro hicho na kura zao kwenye mabano kuwa ni Dalphine Mlewa wa CUF (974), Aloyce Nduguta kutoka Ada Tadea (265), Omari Sombi wa AFP (116) na Mchungaji Yohana Labisu wa CCK (86).
Mandoa alisema wao kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na vyama vya siasa vilivyokuwa vikigombea, walitimiza wajibu na ndipo alipoibuka mshindi kutoka CCM, Justin Monko.
Uchaguzi huo ulifanyika kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Lazaro Nyalandu aliyefukuzwa uanachama wa CCM mwishoni mwa mwaka jana kisha kutimukia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
SONGEA MJINI
Dk Ndumbaro alifanikiwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi kuziba nafasi iliyoachwa baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Leonidas Gama kufariki dunia mwishoni mwa mwaka jana.
Katika uchaguzi huo, Dk Ndumbaro alipata ushindi wa kura 45,162 akifuatiwa na mgombe wa Chama cha CUF aliyepata kura 608, Tadea kura 471, Demokrasia Makini kura 22, CCK 59, TLP 53, NRA 20, AFP 374, UDP 56 na UPDP kura 30.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Songea Mjini, Tina Sekambo, alisema uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu na hivyo kuwapongeza wananchi waliojitokeza kutumia nafasi hiyo kumpata kiongozi wanayempenda.
Wachambuzi, Wanasiasa wanena Mchambuzi wa siasa, Profesa Benson Bana (pichani) anasema kuwa ushindi wa kishindo wa CCM kwenye uchaguzi wa marudio unatokana na jinsi serikali yake ilivyotekeleza mambo yake ndani ya miaka miwili tangu Rais Dk Magufuli alipochaguliwa.
Profesa Bana alisema: “Kwa hali ya sasa ya CCM kwa wananchi ni wazi kuwa walikuwa wanaweza kushinda. Imewapa matumaini makubwa wananchi lakini hii inatokana na jinsi walivyojijengea heshima na kuaminika.
“Lakini ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mdogo si kiashiria kuwa itashinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu. Kwasasa wapiga kura wengi hawavutiwi na kupiga kura kama inavyokuwa kwenye uchaguzi mkuu, pia wengi wamekuwa wakichagua mbunge au mwakilishi ambaye anatoka chama tawala kwasababu huko ndipo kwenye neema yaani timu ya ushindi.”
Kwa upande wa vyama vya upinzani, Mwenyeki wa Chama cha UPDP, Fahim Dovutwa alisema kuwa kuwa CCM imeshinda kutokana na sera bora na kwamba uchaguzi kwao wanaamini kuwa kuna kushinda na kushindwa.
Alisema: “Uchaguzi ni uchaguzi tu, mwenye sera nzuri ndiyo huwa anashinda hivyo siamini kwenye michezo michafu kama kuibiwa na kadhalika kwasababu kiongozi au ushindi wa kiongozi unatokana na Mungu kuridhia.
“Sisi kama wapinzani tunapokea matokeo na hatuna kinyongo kwasababu kuna kushinda na kushindwa,”alisema. Imeandaliwa na Alfred Lasteck, Matern Kayera- Dar, Muhidin Amri-Songea, Abby Nkungu-Singida na John Mhala, Longido.
תגובות