RAIS John Magufuli amekata mzizi wa fitina na kuwataka Watanzania wapuuze mjadala unaoendelea juu ya kuongezwa muda wa urais kutoka miaka mitano hadi saba, akisema ni kinyume cha Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Katiba ya nchi.
Aidha, imebainika kuwa Rais Magufuli hana mpango wowote na hatarajii kuongeza kipindi cha Urais wakati wote wa uongozi wake. Rais Magufuli amemuelekeza Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole kuwajulisha wanachama wa CCM na umma wa Watanzania, kuwa anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala huo ambao umekuwa ukichochewa na baadhi ya wanasiasa katika siku za karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu jana kwa vyombo vya habari, Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Polepole, Ikulu, Dar es Salaam.Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya mazungumzo hayo, Polepole alisema Rais Magufuli amemuelekeza kuwajulisha wanaCCM na umma wa Watanzania kuwa anasikitishwa na hafurahishwi na mjadala unaoendelea juu ya kuongezwa kwa kipindi cha Urais kutoka miaka mitano iliyowekwa kwa mujibu wa Katiba, hadi miaka 7.
“Ndugu Polepole amesema Dk Magufuli amewataka wanachama wa CCM na umma wa Watanzania kwa ujumla kuupuuza mjadala huo, kwa kuwa haujawahi kujadiliwa katika kikao chochote cha chama, na ni kinyume na Katiba ya CCM na Katiba ya nchi,” ilieleza taarifa ya Ikulu.Polepole aliongeza kuwa Rais Magufuli amewataka wanaCCM na umma wa Watanzania kutokubali kuyumbishwa ama kupotoshwa na mambo yasiyokuwa ya msingi na badala yake wajielekeze katika ajenda muhimu ya kujenga uchumi na kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Aidha, Polepole amebainisha kuwa Dk Magufuli hana mpango wowote na hatarajii kuongeza kipindi cha Urais wakati wote wa uongozi wake. Katika siku za karibuni, baadhi ya wanasiasa nchini wakiwamo wabunge wa CCM wamekuwa wakitaka muda wa kutawala kuongezeka kutoka miaka mitano hadi saba, na wengine kumtaja Rais Magufuli aongezewe muda wa utawala.
Mbunge wa Chemba mkoani Dodoma, Juma Nkamia aliwasilisha muswada binafsi bungeni mwaka jana akilitaka Bunge kufanya marekebisho ya Katiba ili kutoa nafasi kwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uwe unafanyika baada ya miaka saba badala ya mitano ya sasa.Nkamia alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano ni gharama kubwa kwa nchi masikini kama Tanzania. Naibu Waziri huyo wa zamani alisema ameamua kupeleka muswada huo binafsi kwa Spika wa Bunge kutokana na serikali kutumia gharama kubwa za kufanya uchaguzi kwa wakati mmoja; ule wa Serikali za Mitaa na ule Mkuu.
“Napeleka hoja au muswada binafsi kwa Spika wa Bunge, tulijadili hili kama linaweza kufanywa sheria lifanyike,” alikaririwa Nkamia akisema mwaka jana na kuwasilisha muswada huo Septemba 12, 2017.
Nkamia alifafanua kuwa hajamlenga rais aliyeko madarakani ndiye aanze kwenda miaka saba, bali ni kwa viongozi wote na kama wazo lake likitimia wakati Rais Magufuli akiwa madarakani nayo si vibaya. Kwa upande wake, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani maarufu Profesa Maji Marefu, naye alitaka Rais Magufuli aongezewe miaka mingine 10 ya kuongoza ili atawale nchi hii kwa miaka 20.
Maji Marefu alitoa kauli hiyo Agosti mwaka jana wakati wa uzinduzi wa stendi mpya ya mabasi katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe uliofanywa na Rais Magufuli, akidai Dk Magufuli anafanya kazi ambayo Watanzania wanaipenda na inaonekana, hivyo itakuwa ni jambo jema kama ataongezewa muda zaidi wa kuongoza.
“Rais Magufuli wewe ni jembe sana na wewe umeletwa na Mungu. Katika watu ambao watasema katika Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambayo mimi ni mjumbe, basi mimi nitasema wewe uongezewe miaka hii miaka kumi haikutoshi, uongezewe miaka ufanye kazi miaka 20 na hilo pendekezo la Ilani ya Uchaguzi lije mapema.
“Mashehe wapo hapa, viongozi wa dini wapo hapa na sisi waganga wa kienyeji tupo hapa, tutakuombea hilo wazo litapita, mtu anayefanya kazi hakuna kumbadilisha badilisha, unafanya kazi ambayo Watanzania wanaipenda tukibadilisha badilisha tunaweza kupata mtu ambaye ataimaliza nchi yetu,” alieleza Majimarefu.
Aidha, Kada wa CCM, Laurence Mabawa alikaririwa mwaka jana akisema kuwa kutokana na shughuli kubwa anayoifanya Rais, ameandaa Kampeni ya ‘Magufuli Baki’ ambayo anatarajia kuzunguka nchi nzima kuwashawishi wananchi kuungana kuliomba Bunge libadilishe vifungu vya Katiba ili kumwongezea muda wa kuongoza.
“Kutokana na mambo makubwa anayoyafanya mimi kama Kada wa CCM anayelitakia mema taifa hili sina budi naungana na Watanzania walio wengi kuanzisha kampeni hii ili kuliomba Bunge katika vikao vyake vijavyo libadilishe baadhi ya vifungu vya Katiba ambavyo vitamwezesha kumwongezea muda wa kuwa madarakani ili atimize ndoto yake ya kuwa na Tanzania iliyo safi,” alisema Mabawa.
Alipotoa maoni yake kuhusu mjadala huo, Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Pius Msekwa alisema CCM hakiwezi kukubaliana na maoni au mpango wa kuongeza muda wa kiongozi yeyote kutoka kipindi cha miaka mitano kilichopo kikatiba kwa sasa.
Msekwa alisema hoja hiyo inabidi iangaliwe kwa umakini mkubwa kutokana na ukweli kuwa, iwapo kiongozi atakuwa mbaya, maisha yanaweza kuwa ya mateso kupitia kiongozi huyo na kuongeza kuwa hilo hata Baba wa Taifa, Julius Nyerere aliliona hilo.
“Ni kwamba miaka kumi tu inatosha, ili kama mtu ni mbaya tuvumilie kwa hiyo miaka kumi, na siyo kwamba haikufikiriwa…na sidhani kama CCM itakuwa na nafasi ya kujadili hilo kwa sasa,” alisema Msekwa
Comments